Yanga yatinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika
Timu ya Yanga, imeweka rekodi ya kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza tangu timu hiyo kuanzishwa kwakwe kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya CR Belouizdad.
Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, umeifanya Yanga kufikisha alama 8 nyuma ya Al Ahly yenye alama 9 huku Belouizdad ikishika hadi nafasi ya pili kwa alama zao 5 na Medeama FC alama 4.
Yanga itamaliza mechi yao ya mwisho ugenini dhidi ya Ahly huku Belouizdad ikiwa nyumbani dhidi ya Medeama.
Mechi hizo hazitaathiri msimamo wa Kundi hilo D hata kama Belouizdad itashinda kwa idadi kubwa ya mabao na kufikisha alama 8 sawa na Yanga ambayo labda itafungwa na Ahly, haitoweza kuishusha timu hiyo kutokana na matokeo yao binafsi timu hizo zilipokutana.
Katika mechi ya kwanza, Yanga ugenini ilifungwa mabao 3-0 lakini katika mchezo wa leo imeshinda mabao 4-0, hivyo ina uwiano mzuri wa mabao na ndio maana imetinga robo fainali.
Katika mchezo huo ambao ulihudhuriwa na maelfu ya mashabiki wao, mabao ya Yanga yalifungwa na Mudathir Yahaya, Stephani Aziz Ki, Kennedy Musonda na Joseph Guede.
Ni mchezo ambao Yanga tangu dakika ya kwanza ilionekana kutaka matokeo kutokana na kufanya mashambulizi ya mara kwa mara huku Belouizdad ilionekana kutaka sare pekee.
Jitihada hizo za Yanga, zilianza kuonekana tangu dakika ya 9 ambapo Musonda alichelewa kuunganisha mpira uliopigwa na Pacome Zouzoua na kutoka nje ya goli.
Mashabiki wa Yanga wakionekana kukata tamaa waliamini watakwenda mapumziko bila bao, ndipo Mudathir alipofunga bao dakika ya 42 akiunganisha krosi iliyopigwa na Joyce Lomalisa.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya kwanza tu, Aziz Ki alifunga bao la pili baada ya kuonana vizuri na Musonda na kupiga shuti lililojaa wavuni.
Ikapita dakika moja nyingine Belouizdad wakiwa bado wana kiwewe, Musonda alifunga bao la tatu baada ya Pacome kuwapiga chenga wachezaji watatu na Kipa wa Belouizdad na kisha kumsetia Musonda aliyekwamisha mpira wavuni.
Zikiwa zimebaki dakika sita kipyenga cha mwisho kupulizwa, Guede ambaye aliingia badala ya Musonda, alifunga bao la nne akiitendea haki pasi ya upendo ya Aziz Ki.
Katika mchezo huo, Belouizdad itajutia nafasi iliyopata dakika ya 45 kupitia kwa Youcef Laouafi ambaye alipiga kichwa ndani ya eneo la hatari na kudakwa na Kipa Djigui Diarra.