Yanga SC yaipiga 5G Polisi Tanzania michuano ya ASFC
Mabingwa wa michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), timu ya Yanga SC, imeendeleza wimbi lao la ushindi katika michuano hiyo kwa kuitandika 5-0 Polisi Tanzania katika mchezo uliopigwa Azam Complex, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Straika mpya wa Yanga, Joseph Guede, aliondoa mkosi kwa kufunga mabao mawili baada ya kucheza michezo mitano tofauti ya mashindano mbalimbali bila kufunga.
Nyota huyo ambaye alisajiliwa katika dirisha dogo kuzina lengo la Fiston Mayele, alionekana kuzua hofu kwa mashabiki wa timu hiyo kutokana na ukame wa mabao aliopitia.
Baada ya kufunga kila bao ndani ya dakika 45 za kwanza, Guede alionekana akishangilia kwa kupangusa jezi yake akiashiria kutoa nuksi.
Mabao mengine katika mchezo huo, yalifungwa na Farid Mussa, Clement Mzize ambaye hadi sasa ana mabao manne katika michuano hiyo na bao la Tano lilifungwa na kinda, Shekhan Rashid kwa mkwaju wa penalti.
Katika dakika 45 za kwanza, Yanga tayari ilikuwa imeshaingia kambani mara tatu kutokana na mabao ya Guede na Farid na kuifanya Yanga kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 3-0.
Ushindi huo, umeifanya Yanga kutinga hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo ambapo sasa itaumana na Dodoma Jiji.
Baada ya mchezo huo, Yanga itaelekeza akili zao katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad, mchezo utakaopigwa Jumamosi Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.