Mudathir aipeleka Yanga SC kileleni Ligi Kuu
Kiungo wa timu ya Yanga SC, Mudathir Yahaya, ameingia kutoka benchi na kufunga bao muhimu ambalo limeipaisha timu yake hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
Mchezo huo namba 103, uliofanyika katika Uwanja wa Azam Complex, ilionekana dhahiri Yanga wanakaribia kupata suluhu ya pili mfululizo ndani ya siku tatu.
Mudathir ambaye alifunga bao hilo dakika ya 86 baada ya kupokea pasi safi ya Nickson Kibabage, aliingia uwanjani kuchukuwa nafasi ya Jonas Mkude ambaye alianza mchezo huo.
Hii sio mara ya kwanza Mudathir kuwafunga Dodoma akiwa na jezi ya Yanga, Mei 12, mwaka jana, mchezaji huyo alifunga mabao mawili ambayo yaliisaidia timu yake kutangaza ubingwa wa ligi kuu.
Yanga licha ya kuutawala mchezo kwa asilimia kubwa lakini tatizo lilionekana dhahiri kwenye eneo lao la mbele ambapo wakati fulani walionekana kupoteza mawasiliano.
Pacome Zouzoua ambaye alipewa nafasi ya kuwa mchezaji huru eneo la mbele alionekana kufanya jitihada nyingi lakini hazikuwa na matunda kwa upande wa timu yake.
Hata hivyo, ukuta wa Dodoma Jiji chini ya Joran Mgeveke na Mtenje Albano, ulifanya kazi ya ziada kuhakikisha Yanga hawapati nafasi kubwa za mara kwa mara.
Nafasi kubwa za Yanga katika mchezo huo ziliwaangukia mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Joseph Guede kipindi cha kwanza na Clement Mzize kipindi cha pili lakini mipira yao ya kichwa yote iliokolewa na Kipa, Mohamed Hussein.
Dodoma Jiji wao hawakutengeza nafasi kubwa katika mchezo huo ambapo Kocha wao, Mike Baraza alionekana kuipanga timu yake katika hali ya uzuiaji zaidi.
Kwa matokeo hayo sasa, Yanga wamekamatia usukani wa ligi baada ya kufikisha alama 34 huku wakiwashusha Azam FC ambao wana alama 31 katika nafasi ya pili.
Yanga mara baada ya mchezo huo watasalia Dar es Salaam na Februari 8 watakuwa tena katika dimba hilo la Azam Complex kucheza na Mashujaa FC kutoka Kigoma.