Mudathir aifungia Yanga SC bao la ushindi ikijikita kileleni
Kiungo Mudathir Yahaya, ameendelea kudhihirisha ubora wake ndani ya Uwanja wa Azam Complex baada ya kufunga tena bao muhimu ambalo limeipatia alama tatu timu yake ya Yanga na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Mudathir kufunga bao la ushindi kwenye dakika za mwishoni akiwa amefanya hivyo katika mchezo uliopita ambapo Yanga ilishinda 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
Yanga sasa kwa matokeo hayo, imezidi kujikita kileleni kwa kukusanya alama 37 wakiwaacha Azam katika nafasi ya pili kwa tofauti ya alama 6.
Mchezo huo ulikuwa ni wa mwisho kwa Ile michezo ya viporo kwa upande wa Yanga ambao sasa wamecheza mechi 14 na wamebakisha mechi moja kama timu nyingine ili kukamilisha duru la kwanza.
Mashujaa ambao katika mechi iliyopita wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Lake Tanganyika, Kigoma, ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Simba, kwenye mchezo huu pia waliingia kwa tahadhari kubwa wakicheza kwa kuwaheshimu Yanga ambao walikuwa na mpira kwa muda mwingi wa kipindi cha kwanza.
Hata hivyo Yanga hawakufanikiwa kufunga bao la mapema na kikwazo zaidi alikuwa ni Kipa, Eric Johora ambaye aliokoa michomo mikali kutoka kwa Pacome Zouzoua, Joseph Guede na Clement Mzize.
Zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya mapumziko, Max Nzengeli alifunga bao la kwanza katika mchezo huo akimalizia mpira uliotemwa na Johora baada ya kuokoa shuti lililopigwa na Mzize.
Hilo lilikuwa ni bao la kwanza kwa Nzengeli na la nane msimu huu baada ya kupita mechi tano tangu mara ya mwisho alipofunga kwenye mechi dhidi ya Simba, Novemba 5, mwaka jana.
Kipindi cha pili Mashujaa walikuja kwa kasi na mabadiliko yaliyofanywa na Kocha, Mohamed Bares yalizaa matunda sekunde chache tu baada ya Emanuel Mtambuka kufunga bao la kusawazisha akitumia mpira wake wa kwanza kugusa tangu alipoingia.
Kusawazishwa kwa bao hilo, kuliifanya Yanga kuinuka zaidi na kufanikiwa kufunga bao hilo la ushindi zikiwa zimesalia dakika mbili mpira kuisha.
Yanga sasa watahamishia akili zao mkoani Mbeya ambapo Februari 11 itacheza dhidi ya Tanzania Prisons.