Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), imeizuia timu ya Chippa United inayoshiriki Ligi Kuu nchini Afrika Kusini, kusajili hadi itakapomlipa mchezaji Abdi Banda randi 1,200,000 (zaidi ya sh. milioni 120 za Kitanzania).
Adhabu hiyo imetolewa baada ya Mtanzania Banda kushinda kesi yake ya madai aliyoiwasilisha dhidi ya waajiri wake hao wa zamani.
Kwasasa Banda ameungana na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kwa ajili ya mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Niger na Morocco.
Banda bado anacheza Ligi ya Afrika Kusini na sasa hivi anakitumikia kikosi cha Richards Bay FC.
Hili ni pigo kwa Chippa United ambao hawapo vizuri kwenye msimamo wa ligi na kama hawatoweza kulipa fedha hizo kwa wakati basi watashindwa kuboresha kikosi chao kwenye usajili wa Januari.
Banda alishawahi kuzichezea timu za Simba SC, Coastal Union na Mtibwa Sugar za Tanzania na kisha kusajiliwa na Baroka FC, Highlands Park zote za Afrika Kusini.