Taifa Stars yapigwa 3-0 na Morocco AFCON
Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', imeanza vibaya michuano ya Afcon kwa kutokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Morocco.
Mchezo huo wa kwanza kwa kila timu katika Kundi F ulichezwa katika Uwanja wa Laurent Pouk.
Morocco ambayo ni timu namba moja kwa ubora Afrika, waliingia katika mchezo huo wakiwa wanapewa nafasi kubwa ya kushinda na walifunga bao la kwanza dakika ya 30 ya mchezo kupitia kwa nahodha wao, Romain Saiss.
Matokeo hayo yalibaki hadi mapumziko huku Stars chini ya Kocha, Adel Amrouche walionekana kutokuwa na mpango wowote mzuri wa kupata bao.
Kipindi cha pili kiliendelea kwa Stars kuendelea kucheza kwa muda mwingi wakiwa katika eneo lao na kuwapa nafasi Morocco kutawala mchezo kwa asilimia kubwa.
Katika dakika ya 70 ya mchezo, kiungo wa Stars, Novatus Dismas alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano.
Kutoka kwa Dismas kuliidhoofisha zaidi Stars na walijikuta wakiruhusu mabao mawili ya haraka yalioyofungwa na Azzedine Ounahi na Youssef En-Nesyri.
Kuingia kwa mabao hayo, kuliwafanya Stars kupoteana zaidi na kama si uimara wa mlinda lango, Aishi Manula basi matokeo yangekuwa mabaya zaidi.
Mara baada ya mchezo huu Stars, watashuka tena dimba Januari, 21 kucheza dhidi ya Zambia ambao nao walitarajia kucheza dhidi ya DR Congo usiku wa kuamkia leo.
Kikosi cha Stars kilichoanza: Aishi Manula, Hajj Mnoga, Mohamed Hussein, Bakari Nondo, Ibrahim Abdullah, Novatus Dismas, Himid Mao, Mudathir Yahaya, Charles M'mbobwa, Mbwana Samatta na Tarryn Allarakhia.