Simba SC yaipiga Tembo FC 4-0 michuano ya ASFC
Mshambuliaji mpya wa Simba ambaye alisajiliwa kwenye dirisha dogo, Pa Omar Jobe, ameanza maisha yake ndani ya Tanzania kwa kishindo baada ya kufunga bao moja na kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tembo FC kwenye mchezo wa Azam Sports Federation Cup (ASFC).
Katika mchezo huo ambao ulifanyika katika Uwanja wa Azam Complex, Jobe, alifunga bao hilo kipindi cha pili baada ya kuingia akitokea benchi.
Usajili wa Jobe ambaye ni raia wa Gambia, ulizua gumzo nchini Tanzania hasa baada ya kutajwa kuchukuwa nafasi ya Jean Baleke ambaye alikuwa ni kipenzi cha mashabiki wa Simba.
Simba ambao walionekana kuutawala mchezo huo kuanzia mwanzo, walifunga mabao mawili kipindi cha kwanza kupitia kwa Luis Miquisonne na Saido Ntibanzokiza.
Bao lingine katika mchezo huo, lilifungwa na Saleh Karabaka ambaye naye alisajiliwa katika dirisha dogo la usajili akitokea JKU.
Hii ni mara ya pili kwa Karabaka kufunga katika michuano mbalimbali akiwa na jezi ya Simba, mara ya kwanza alifunga bao moja kwenye mechi dhidi ya JKU wakati wa michuano ya Mapinduzi Cup.
Mbali na Jobe na Karabaka ambao walifunga mabao lakini pia Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha, alimuingiza kikosini Ladack Chasambi huku Freddy Michael Koublan na Edwin Balua wao wakipata nafasi ya kuanza.
Mara baada ya mchezo huo Kocha Benchikha, alisema amefurahia kiwango cha timu yake katika mchezo huo na kwamba wameitumia mechi hiyo kama sehemu ya maandalizi kuelekea michezo ya Ligi Kuu Bara.
"Mechi ilikuwa nzuri, nashukuru kwa ushindi huu lakini kubwa zaidi nimefurahishwa na kiwango cha timu yetu, mechi hii ni maandalizi mazuri kuelekea mechi zetu za ligi kuu," alisema.
Mara baada ya mchezo huo, Simba watahamishia akili zao katika michuano ya ligi ambapo Januari 3 watashuka Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma kucheza dhidi ya Mashujaa FC.