Mzize apiga 'hat trick' Yanga ikiua 5-1 ASFC
Mabingwa watetezi wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam, timu ya Yanga SC, imeanza kwa kishindo kampeni yao ya kulitetea taji lao kwa kuwatandika Hausung FC ya mkoani Njombe kwa jumla ya mabao 5-1.
Shujaa katika mchezo huo alikuwa ni Clement Mzize ambaye alifunga mabao matatu 'hat trick' na kuwa mmoja kati ya wafungaji vinara katika michuano hiyo hadi sasa.
Mzize alifunga mabao yake katika vipindi viwili tofauti ambapo kwenye kipindi cha kwanza alifunga mabao mawili na bao lingine alifunga kwenye kipindi cha pili kabla ya kufanyiwa mabadiliko.
Mabao mengine kwa upande wa Yanga yalifungwa na Mahlatse Makudubela 'Skudu' huku lingine likifungwa na Jonas Mkude.
Mchezo huo ambao dhahiri ulionekana kuwa wa upande mmoja uliendelea kushuhudiwa Yanga wakitengeneza nafasi nyingi ambazo nyingine walishindwa kuzitumia.
Bao la kufutia machozi kwa upande wa Hausung ambao ni mabingwa wa Mkoa wa Njombe, lilifungwa na Tony Jailos ambaye katika michuano hiyo msimu huu amefikisha bao la tatu.
Kipindi cha pili, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, aliwapa nafasi ya kucheza wachezaji Pacome Zouzoua, Kouassi Yao, Wilson Chigombo, Nickson Kibabage na Denis Nkane ambao wote walianzia nje.
Katika mchezo huo, Yanga pia walitumia nafasi ya kumtambulisha mshambuliaji wao mpya Joseph Guede raia wa Ivory Coast ambaye alijiunga na timu kwenye dirisha dogo la usajili.
Mara baada ya mchezo huo, Yanga sasa watahamishia akili zao katika michuano ya Ligi Kuu Bara ambapo kesho kutwa kikosi kitashuka tena uwanjani ugenini kwenye dimba la Kaitaba, kucheza na Kagera Sugar.
Michuano hiyo ya FA mzunguko wa pili inahitimishwa kesho, kwa Simba SC kuwavaa Tembo kutoka Tabora.
Mchezo huo utachezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na unatarajia kuanza saa 1 usiku.
Mechi nyingine itakuwa ni kati ya wenyeji Kagera Sugar ambao watakuwa kwenye uwanja wa Kaitaba kucheza dhidi ya Dar City.