Advertisement
KANDANDA

Msuva afikia rekodi ya mabao ya Samatta Taifa Stars

Mshambuliaji wa Taifa Stars, Simon Msuva
Nyota huyo alifunga bao pekee katika mchezo uliomaliza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia
Advertisement

Bao pekee lililofungwa na mshambuliaji, Simon Msuva, limeisaidia timu yake ya Taifa ya Tanzania ' Taifa Stars', kupata sare ya pili kwenye michuano ya AFCON tangu ianze kucheza ikitoka 1-1 na Zambia.

Advertisement

Msuva ambaye kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake kuvunjwa na JS Kabylie ya Algeria, amefikisha mabao 23 sawa na nahodha wake, Mbwana Samatta katika upachikaji mabao wa muda wote ndani ya Stars.

Kinara wa mabao ndani ya taifa hilo, ni Mrisho Ngassa ambaye amefunga mabao 25.

Stars hizo ni fainali zake za tatu tangu ianze kushiriki na huo ni mchezo wao wa nane lakini bado haijafanikiwa kuondoka na alama 3.

Sare ya kwanza walipata mwaka 1980 waliposhiriki kwa mara ya kwanza nchini Nigeria ambapo walitoka 1-1 na Ivory Coast.

Advertisement

Matokeo ya mchezo huo, yanawafanya Stars kuendelea kukaa mkiani mwa kundi hilo ambalo sasa linaongozwa na Morocco wenye alama 4 baada ya wao pia kulazimishwa sare ya 1-1 na DR Congo katika mchezo uliochezwa mapema.

Stars ambayo ilikuwa chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Hemed Morocco, walionekana kuimarika kimchezo tofauti na walivyocheza dhidi ya Morocco kwenye mechi ya kwanza na walifunga bao la mapema katika dakika ya 11 kupitia kwa Msuva.

Wakati mchezo huo ukiwa chini ya utawala wa Stars, Zambia walijikuta katika mshangao mwengine kwenye kipindi hicho cha kwanza baada ya nahodha wao, Roderick Kabwe kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kadi mbili za njano.

Mara baada ya kadi hiyo, Stars walionekana kuridhika na kuanza kucheza taratibu huku walipoteza mipira mingi bila sababu za msingi.

Kipindi cha pili kiliendelea kwa utulivu huku Zambia walionekana kucheza kwa mbinu zaidi hasa za kushambulia kwa kushtukiza.

Advertisement

Mabadiliko ya Kocha wa Zambia, Avram Grant kumuingiza mchezoni Claotus Chama na Kennedy Musonda yalionekana kuwongezea kasi zaidi Zambia na kusawazisha bao dakika ya 88 kupitia kwa mshambuliaji wao, Patson Daka ambaye anacheza Leicester City ya Uingereza.

Stars sasa wanahitajika kushinda kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya DR Congo, Januari 24 ili kuweza kuweka hai matumaini ya kufuzu hatua ya 16 Bora.

Advertisement
Loading discussion…

Signing in with Google...